Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kwa kushirikiana na Taasisi ya kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) wamefanikiwa kupata mbegu za malisho zenye sifa ya kustawi na kufanya vizuri kwa upande wa afya na lishe ya mifugo iliyopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Dkt. Jonas Kizima wakati wa uzinduzi wa majaribio ya upandaji mbegu za malisho aina ya “Brachiaria” uliofanyika kwenye mashamba ya Ofisi za Taasisi hiyo kituo cha Mpwapwa Mkoani Dodoma ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo imetokana na utafiti wa muda mrefu ambao taasisi yake ilifanya kutoka mikoa 20 ya hapa Tanzania bara ili kupata aina mbalimbali za aina hiyo ya mbegu za malisho yanayoweza kustahimili hali ya tabia nchi.
“Kuanza kutumika kwa mbegu hizi kutaisaidia nchi kupunguza utegemezi wa kuagiza mbegu za malisho kutoka nje ya nchi ambapo kwa maeneo yenye ukubwa wa hekta Milioni 2.8 ambayo nchi imeyatenga kwa ajili ya malisho yanahitaji takribani tani 7 za mbegu za malisho ambazo kama zikinunuliwa nje ya nchi zitagharimu dola za Marekani 280” Dkt. Kizima
Dkt. Kizima ameongeza kuwa utafiti wa Taasisi yake ulibaini zaidi ya aina 279 za mbegu aina ya brachiaria ambazo kupitia taasisi ya utafiti wa kimataifa ya Utafiti wa mifugo zilipelekwa kwenye maabara ya taasisi hiyo na kufanyiwa tathmini ya vinasaba vya aina hiyo ya mbegu.
“Baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo zilipatikana aina 10 za aina hiyo ya mbegu na sasa tutasambaza aina hizi za mbegu kwenye vituo vinne ambavyo ni kituo cha Tanga (Ukanda wa chini), kituo cha Mpwapwa (Kanda ya kati/Nyanda kame), kituo cha Mabuki (Kanda ya ziwa) na kituo cha Uyole (Kanda ya nyanda za juu kusini) ili kubaini ni aina ipi inafaa katika ukanda upi ili ile itakayokubaliwa na wakala wa urasimishaji mbegu (TOSCH) tuwape wazalishaji wa mbegu hapa nchini waanze kuzalisha kibiashara” Dkt. Kizima.
Akiainisha faida za aina hiyo ya mbegu za malisho, Dkt. Kizima amesema kuwa mbegu hizo zina faida na sifa nyingi zaidi ukilinganisha na aina nyingine ya mbegu ikiwa ni pamoja na kustahimili ukame, kuwa na virutubisho vingi zaidi vya protini na uwezo wa kuzalisha hadi tani 14 kwa hekta wakati aina nyingine za mbegu zikiwa na uwezo wa kuzalisha hadi tani 9 tu kwa hekta.
Akizungumzia kuhusiana na tafiti mbalimbali zinazofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI), Mkurugenzi wa Utafiti, mafunzo na ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Angelo Mwilawa amesema kuwa matokeo ya utafiti huo ni sehemu ya tafiti mbalimbali ambazo Wizara imekuwa ikizifanya ili kuboresha mazingira kwa wafugaji waliopo nchini.
“ Tafiti hizi zinafanyika ili kuhakikisha kwamba lishe inayopatikana kwa mifugo inakuwa ni yenye tija na ya gharama nafuu ili kumfanya mfugaji yoyote aweze kumudu katika mazingira anayofanyia shughuli zake” Dkt. Mwilawa.
Uwepo wa tafiti zinazolenga kuongeza tija kwa mfugaji hapa nchini ni sehemu ya utekelezaji wa Ajenda ya Utafiti wa Mifugo ya mwaka 2020/2025 ambayo imelenga kufanyia kazi vipaumbele vya kitaifa vya wadau wote wa sekta ya mifugo nchini.