Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeishauri Serikali kuongeza bajeti ya usimamizi wa masuala ya usalama na afya ili kuuwezesha Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuzuia ajali, magonjwa na uharibifu wa mali katika shughuli za uzalishaji hususan miradi mikubwa ya maendeleo jambo ambalo litaongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi nchini.
Ushauri huo umetolewa mara baada ya OSHA kuwasilisha randama ya bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 pamoja na taarifa ya muundo na majukumu yake mbele ya Kamati hiyo Bungeni Jijini Dodoma.
Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ndiyo inayoisimamia Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi chini yake ikiwemo OSHA kwasasa.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Riziki Saidi Lulida, amesema OSHA ina jukumu kubwa la kusimamia mifumo ya kuzuia ajali na magonjwa katika maeneo ya kazi hivyo kupelekea shughuli za uchumi kufanyika kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Kiongozi huyo wa Kamati ameongeza kuwa kutokana na jukumu hilo zito la OSHA, Serikali haina budi kutenga bajeti ya kutosha ili kuiwezesha OSHA kufanya kazi yake ipasavyo hususan katika miradi mikubwa ya mafuta na gesi ambayo inahitaji kushughulikiwa kwa umakini mkubwa ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kutokea endapo ajali zitatokea katika maeneo husika.
“Uwepo wa OSHA ni mkakati wa maendeleo ya wafanyakazi na usalama wa nchi lakini watu wengi wanakwepa kutekeleza taratibu za usalama na afya kwenye maeneo ya kazi. Hivyo, sisi tunaishauri serikali isimame imara na iwape OSHA bajeti ya kutosha ili waweze kufanya kazi ya kuisaidia nchi katika eneo la usalama wa wafanyakazi katika viwanda vyetu, Taasisi zetu, mabomba yetu ya mafuta na gesi, mashirika ya umma na makampuni binafsi,” ameeleza Mbunge Lulida.
Aidha, Kamati hiyo imebainisha kwamba OSHA imeleta mabadiliko makubwa katika usimamizi wa masuala ya usalama na Afya katika shughuli mbali mbali za uzalishaji mali ikiwemo sekta ya Mafuta na Gesi.
“Mafanikio ya OSHA ni makubwa sana endapo tukiangalia tulikotoka ambapo wafanyakazi walikuwa hawajui haki zao za msingi kuhusiana na masuala ya usalama na afya mahali pa kazi. Mathalani katika vituo vingi vya mafuta tulikuwa tunaona vijana wakitoa huduma bila kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa kinga kama vile viatu maalum vya usalama (safety boots) badala yake walikuwa wanavaa ndala au lakini sasa hali imebadilika na vituo vingi wanazingatia taratibu muhimu za usalama na afya,” amesema Mariamu Kisangi, Mjumbe wa Kamati.