Naibu Waziri wa Habari, utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis mwinjuma amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya kasi ya teknolojia hasa kwa maudhui yanayopitia kwa watoa huduma za intaneti ambapo kwa kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kutoa leseni za maudhui mtandaoni kwa maombi ambayo yanakidhi vigezo vilivyowekwa.
Mhe. Mwinjuma ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma leo tarehe 3 2025 wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum, Tauhida Gallos aliyetaka kujua namna Serikali imejipanga kuhakikisha ongezeko la vyombo vya Habari Mtandao haliathiri maadili na Utamaduni wa Taifa letu.
Amesema kuwa Serikali imekuwa ikiwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni watengenezaji wa maudhui mtandaoni wanaokiuka sheria na kanuni za utangazaji ikiwemo uvunjifu wa maadili.
“suala la kuzingatia maadili na utamaduni wa taifa letu ni suala mtambuka na huanzia ngazi ya familia, shuleni na jamii yetu kwa ujumla. Hivyo, kila mwananchi kwa nafasi yake anapaswa kuwa mlinzi na msimamizi wa maadili na utamaduni wa taifa letu.” Amesema Mhe. Mwinjuma.