Jeshi la anga la Nigeria limeeleza kuwa lilifanya shambulizi la anga dhidi ya Waasi katika maeneo ya Zurmi na Maradun, Jimboni Zamfara lakini kwa bahati mbaya, shambulizi hilo limesababisha vifo vya raia waliokuwa wakifanya kazi za kijamii za ulinzi katika eneo hilo ambapo tukio hili likiripotiwa kuwa la tatu la aina hii kutokea katika kipindi cha mwaka mmoja.
Aidha Msemaji wa Gavana wa Zamfara, Sulaiman Bala Idris amrsema kuwa mashambulizi hayo yalilenga Waasi waliokuwa wakikimbia lakini baadhi ya Wanachama wa Civilian Joint Task Force na Walinzi wa Vijiji walichukuliwa kimakosa kuwa ni Waasi ambapo Idris alielezea masikitiko yake kwa vifo vilivyotokea na kusema kuwa Watu hao walilengwa kimakosa.
Ingawa Maafisa wa Serikali hawajatangaza idadi rasmi ya vifo, Mashuhuda wanasema walihesabu miili ya Watu 20 huku wengine 10 wakipokea matibabu kwa majeraha.
Mashambulizi ya anga yamekuwa sehemu ya mikakati ya kijeshi ya Nigeria kupambana na Waasi na Makundi ya itikadi kali lakini ripoti zinaonyesha kuwa mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya Raia 400 tangu mwaka 2017, kulingana na utafiti wa SBM Intelligence.
Hali hiyo imejiri baada ya tukio lingine la kimakosa mwezi Desemba 2023, ambapo zaidi ya raia 80 waliuawa katika mkusanyiko wa kidini huko Kaduna ambapo Jeshi la Nigeria lilitangaza kuwa Wanajeshi wawili wangepelekwa Mahakamani kwa tukio hilo lakini matokeo ya uchunguzi bado hayajatolewa hadharani jambo ambalo limekosolewa na Makundi ya haki za Binadamu kwa ukosefu wa uwazi.