Kwa mujibu wa kamati ya upinzani ya Abu Gouta, raia 40 wa kawaida wameuawa katika shambulizi lililofanywa na Kikosi cha Msaada wa Haraka RSF dhidi ya kijiji kimoja, katikati ya Sudan.
Kamati hiyo ambayo ni shirika lisilo la kiserikali imetoa taarifa ikisema, shambulizi la kikosi cha RSF dhidi ya kijiji cha Gouz Al-Naqa cha eneo la Abu Gouta jimboni Gezira limesababisha vifo vya watu zaidi ya 40.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, miili kadhaa iliachwa tu katika kijiji hicho, huku kikosi cha RSF kikiwazuia wanakijiji waliokimbia kurudi kuzika miili hiyo.
Kamati hiyo imetoa mwito kwa asasi za kijamii kushinikiza kikosi hicho kuwaruhusu wakazi kuingia katika kijiji hicho na kuzika miili hiyo.