Mswada wa kuanzisha mchakato wa kuelekea uchaguzi unaosubiriwa kwa muda mrefu nchini Sudan Kusini umezua maandamano bungeni nchinin Sudan Kusini.
Mrengo wa chama tawala nchini humo ulitoka nje ya ukumbi wakati sheria hiyo ikipitishwa.
Wabunge walimshutumu Rais Salva Kiir kwa kukiuka masharti ya mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka wa 2018.
Wabunge hao wa chama cha SPLM, wamemtuhumu spika wa bunge Jemma Nunu Kumba kwa kushinikiza kupitishwa mswada huo wa uchaguzi ambao wamesema matokeo yake yatakuwa ni uchaguzi usio wa demokrasia ,haki na wa kuaminika.
Mswada huo, kwa mujibu wao, umempa mamlaka zaidi rais kufanya uteuzi wa wabunge zaidi hivyo kuwanyanganya raia haki yao.
Rais Kiir amesisitiza uchaguzi huo utafanyika Disemba 2024, ingawaje umoja wa mataifa una wasiwasi kuhusu mazingira salama ya kufanyika uchaguzi huu.
Rais Kiir anatarajiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York baadaye.
Anatarajiwa kuangazia dhamira yake ya kutekeleza makubaliano ya amani.