Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema katika mwaka 2023/2024, shilingi bilioni 743.7 zimetolewa kwa wanufaika zaidi ya milioni sita kupitia mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Ameyasema hayo leo jioni (Jumatatu, Aprili 15, 2024) Bungeni, jijini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025.
“Serikali imeendelea kutekeleza sera mbalimbali za uwezeshaji wa makundi maalum ya wanawake, vijana na wenye ulemavu. Lengo likiwa ni kuhakikisha makundi haya yanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hapa nchini.”
Amesema katika kutekeleza sera ya ushirikishwaji wa Watanzania kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji nchini, wanawake na vijana wameendelea kunufaika kupitia miradi ya kimkakati na uwekezaji ambapo katika mwaka 2023/2024, Watanzania 162,968 wamenufaika na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
“Serikali imeendelea kuratibu masuala ya uzalishaji wa fursa za ajira nchini kwa kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, fursa za ajira 2,489,136 zimezalishwa sawa na wastani wa ajira mpya 829,712 kwa mwaka,” amesema.
Kuhusu vijana, Waziri Mku amesema Serikali imeendelea kuwawezesha vijana ili waweze kujiari, kushiriki kwenye shughuli za maendeleo na kuchangia katika Pato la Taifa. “Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, shilingi bilioni 3.19 kimetolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambazo zilitumika kutoa mikopo ili kuwezesha miradi 148 katika sekta za kilimo, viwanda na biashara katika halmashauri 62.”
Amesema Serikali imetoa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi, kurasimisha na kuendeleza biashara kwa vijana katika maeneo mbalimbali nchini. Ambapo hivi karibuni, Ofisi ya Rais – TAMISEMI itatoa taarifa ya mfumo utakaotumika kutoa mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri nchini.