Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) kwa kushirikiana na Taasisi ya Uwezeshaji Vijana ya StartHub Africa kupitia programu ya ‘YouthIgnite Student Founders Fellowship’ imefanya uwezeshaji wenye thamani ya shilingi milioni 80 kwenye miradi 20 ya kibunifu ya biashara za wanafunzi kutoka vyuo vikuu 10 nchini.
Uwezeshaji huo umefanyika baada ya miradi hiyo kuonekana kuwa na tija katika jamii, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa watu wengine kupitia mnyororo wa thamani wa miradi hiyo.
Akizungumza mkoani Dar es Salaam wakati wa hafla ya uwasilishwaji wa miradi hiyo, Meneja wa Mradi wa Funguo kutoka UNDP, Joseph Manirakiza amesema fedha hizo ni kwa ajili ya bunifu hizo kupata mitaji ya kuanzia, hatua ambayo itawasaidia vijana hao kujiajiri wakiwa vyuoni na kupunguza changamoto ya ajira.
Kwa upande wake, Mwanzilishi wa StartHub Africa nchini Tanzania, Shakila Mshana amesema programu ya ‘YouthIgnite Student Founders Fellowship’ ilifanyika kwa kufanya mchakato wa kutafuta biashara hizo vyuoni ambapo vigezo vilijikita katika biashara zinazoendeshwa na wanafunzi ambao bado wapo vyuoni.
Baadaye waliweka kambi kisha wanafunzi hao wakanolewa kitaalamu kwa wiki nzima, kisha wakawasilisha kazi zao na washindi kuibuka huku wakijizolea mitaji ya biashara zao.
Miradi ya biashara za wanafunzi zaidi ya 30 ilishindanishwa, huku 20 ikiwa ni katika nyanja za kidijitali ambapo miradi ya kuongeza thamani mazao ya kilimo na usafirishaji ni miongoni mwa miradi iliyoibuka na ushindi.