Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambalo leo limezifungia Baa za wazi zaidi ya 80 limesema ndani ya siku 14 Watu waliofungiwa Baa zao wasipolipa faini walizopigwa watafungiwa kabisa leseni zao za biashara.
Akiongea wakati wa Mkutano na Wadau wa Mazingira Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka amesema “Haturudi nyuma, lipa faini uliyopigwa ndani ya siku 14 uendelee na biashara, kama haujalipa tunaandika barua kwa wanaohusika ya kufuta leseni ya biashara”
“Wanaotaka wafunguliwe kwanza walipe faini ya Tsh. Milioni 5 ndani ya siku 14 na waandike barua za kukiri kosa na kuahidi kutorudia makosa ya kuwapigia Watu kelele zilizovuka viwango na watoe ahadi ya kujenga miundombinu ya kudhibiti kelele ndani ya siku 30”
“Pia wanapaswa kufuata masharti ya leseni kama vibali vyao vinavyoelekeza, ukitekeleza haya tunakuandikia barua ya kukuruhusu kuendelea na biashara yako lakini pia tutaendelea kukufuatilia”
“Ukishindwa kutekeleza haya tunakufungia leseni ya biashara, tunaamini mmepata fundisho hamtoweza kuzidi DB 40 hasa wakati wa usiku wakati Watu wakiwa wamelala”