Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha Rais mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi kilichotokea jana.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, katika kipindi hiki cha maombolezo ya kitaifa bendera zitapepea nusu mlingoti.
Nina huzuni kutangaza kifo hiki,” amesema Rais Samia Suluhu Hassan, na kuongeza kuwa rais huyo wa zamani alikuwa akitibiwa saratani ya mapafu. Mwinyi alilazwa London Novemba 2023 kabla ya kurejea kuendelea na matibabu Dar es Salaam, ameongeza Rais wa Tanzania.
Rais Samia ameongeza kuwa, kiongozi huyo aliyeleta mabadiliko ya kidemokrasia Tanzania, atazikwa hapo kesho Jumamosi huko Unguja Zanzibar.
Mwinyi alichaguliwa na mwanzilishi wa taifa la Tanzania Julius Kambarage Nyerere kama mrithi wake, na alichukua uongozi wa nchi iliyokuwa katika mgogoro wa kiuchumi, kufuatia majaribio ya kisosholisti ya miaka kadhaa yaliyofeli.
Mwinyi aliondoa vikwazo katika biashara za kibinafsi na kulegeza sheria za ununuzi wa bidhaa kutoka nje, jambo lililompelekea kupewa jina la utani, “Mzee Rukhsa.”