Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) imesema katika ripoti ya leo, Jumatatu kwamba uagizaji wa silaha wa nchi za Ulaya uliongezeka kwa kasi katika mwaka uliopita kutokana na vita vya Ukraine, na kwamba nchi hiyo yaani Ukraine, imekuwa ya tatu kwa kununua kwa wingi zaidi silaha duniani 2022.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo, uuzaji wa silaha wa Marekani duniani pia umeongezeka kutoka 33% hadi 40%, na ndiyo muuzaji mkubwa zaidi wa silaha duniani katika miongo mitatu iliyopita, ikifuatiwa na Russia.
Taasisi hiyo imeeleza kuwa nchi za Ulaya wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO inayoongozwa na Marekani, zimeongeza ununuzi wa silaha kutoka nje kwa asilimia 65 ikilinganishwa na kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Peter de Weizmann, mtafiti mkuu katika Mpango wa Usafirishaji wa Silaha wa taasisi ya SIPRI anasema japokuwa uagizaji wa silaha umepungua duniani kote, lakini usafirishaji wa silaha kwenda Ulaya umeongezeka kwa kasi kutokana na mvutano kati ya Russia na nchi nyingine nyingi za Ulaya, baada ya mashambulizi ya Russia nchini Ukraine.”
Ukraine kwa sasa inaagiza kiasi kikubwa cha silaha kutoka Marekani na Ulaya, ikishika nafasi ya tatu duniani.
Russia imekuwa ikizilaumu nchi za Magharibi hususan Marekani kwamba ndizo zinazochochea moto wa vita vya Ukraine kwa kuendelea kutuma misaada ya silaha huko Kiev.