Kutokana na vitendo vya ukatilia vinavyoendelea kukithiri nchini Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Taifa (SMAUJATA) imewataka Watanzania kuwa na moyo wa ustahimilivu wanapokutwa na changamoto mbalimbali badala ya kuchukua maamuzi yanayoweza kuigharimu jamii katika maisha.
Wito huo umetolewa na mkurugenzi wa uenezi,vijana na michezo wa Jumuiya hiyo Ndugu Johnson Mgimba hii leo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Njombe ambapo amesema kukosekana kwa ustahimilivu ni miongoni mwa sababu zinazopelekea vitendo visivyofaa ikiwemo ukatili na mauaji.
“Zipo sababu zinazopekea haya mambo kutokea katika jamii yetu,mauaji hayatokeitu kuna sababu kubwa ambayo inakuwa ipo nyuma,inaweza kuwa ukatili wa kingono,kibiashara na wakati mwingine wa kijinsia sasa Mh Rais alikua na 4R kwenye ulimwengu hasa wa kisiasa watu wawe na maridhiano,ustahimilivu ili kujenga jamii yetu na sisi tumeomba ile 4R tuilete kwenye maisha yetu ya kila siku baina ya ndugu na ndugu au jamii ili tuweze kuyanusuru haya mambo ya ukatili”amesema Mgimba
Aidha Mgimba amesema Jumuiya hiyo inaona jitihada za mko wa Njombe katika kupambanana na maswala ya mbalimbali ikiwemo ukatili ambapo pia kupitia waraka maalumu wa mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka kuhusu Udumavu,Ukatili wa kijinsia na matukio ya mauaji umeonyesha kusikitishwa na ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia na mauaji kwenye baadhi ya maeneo ya mkoa huo jambo ambao SMAUJATA imekuwa na imani ya kuwa waraka huo utakwenda kusaidia kupunguza vitendo hivyo.