Top Stories

Hasara ya Bil 2,yampeleka gerezani Kisena wa UDART na wenzake(+video)

on

Mkurugenzi wa UDART, Robert Kisena(46) na wenzake watatu wamesomewa mashitaka 19 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikiwemo utakatishaji fedha wa Mil.603 na kuisababishia hasara UDART ya Bil.2.41.

Mbali ya Kisena, washitakiwa wengine ni Kulwa Kisena(33), Charles Newe(47) na Cheni Shi (32).

Katika makosa hayo, moja ni kuongoza uhalifu, kujenga kituo cha mafuta bila kibali, kuuza mafuta sehemu zisizoruhusiwa, wizi wakiwa Wakurugenzi, utakatishaji fedha manne, kughushi manne, kutoa nyaraka za uongo manne, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu mawili na kuisababishia mamlaka hasara moja.

Washitakiwa hao wamesomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali, George Barasa, Moza Kasubi na Imani Mitumezizi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Miongoni mwa makosa hayo ni utakatishaji fedha linamkabili Robert Kisena na Shi, ambapo wanadaiwa kati ya May 26, 2016 wakiwa NMB Bank Ilala kwa pamoja wakiwa Wakurugenzi wa Longway Engineering huku Kisena akiwa Mkurugenzi wa UDART walifanya muamala wa Mil.603  huku wakijuwa fedha ni zao la kosa la kughushi.

Katika kosa jingine ni kujenga kituo cha mafuta bila kuwa na vibali vya EWURA ambapo linamkali Robert na Kulwa Kisena ambapo wanadaiwa walilitenda January 1, 2015 na December 31, 2017 maeneo ya Jangwani Ilala.

Inadaiwa wakiwa Wakurugenzi wa Kampuni ya Zenon Oil na Gas Ltd kwa pamoja walijenga kituo hicho cha mafuta bila kuwa na kibali cha EWURA.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote na upelelezi bado haujakamilika. Kesi imeahirishwa hadi February 23, 2019 washitakiwa wamerudishwa rumande kwa sababu kesi yao haina dhamana.

VIDEO: WAMBURA AKIPELEKWA GEREZANI, HATIMA YAKE FEBRUARI 14

Soma na hizi

Tupia Comments