Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameishauri Serikali kuwarejesha kazini Walimu wakuu wa Shule za Msingi zilizopo Tunduma Mkoani Songwe waliovuliwa vyeo baada ya kusambaa kwa video ikiwaonesha Wanafunzi wakicheza wimbo wa Msanii Zuchu uitwao ‘Honey’.
Spika amesema kama Walimu hao hawakuwepo Shuleni wakati wa tukio linatokea na Mamlaka ya nidhamu imechukua hatua kabla ya kuwasikiliza iwarejeshe kwenye nafasi zao na kama walikuwepo Mamlaka iendelee na utaratibu wake.
Hoja hiyo imeanza kwa kuibuliwa na Mbunge wa Viti Maalum, Husna Sekiboko aliyehoji kuhusu nyimbo zinazostahili kupigwa kwenye Taasisi za Elimu na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na kuiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutoa mwongozo wa nyimbo gani zinastahili kupigwa na zipi hazistahili.
Akijibu hoja hiyo leo November 6 2023 , Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema nyimbo ambazo hazistahili kupigwa kwenye Taasisi za Elimu ni pamoja na zile zinazohamasisha ngono, ulevi au sigara aidha ameongeza kuwa sio kila kinachokubaliwa uraiani kinakubaliwa Shuleni na kama Wizara ina wajibu wa kusimamia suala hilo.