Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumuhoji mshtakiwa Alloyscious Mandago katika kesi ya kuisababishia Serikali hasara ya Shilingi. Bil 2 inayomkabili yeye na wenzake wanne akiwemo mfanyabiashara aliyetajwa na Rais John Magufuli akiiba Sh. Milioni 7 kwa dakika, Mohamed Yusufali.
Maombi hayo yamewasilishwa na Wakili wa Takukuru, Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Swai amedai kuwa wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha taarifa ili kuwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi pia ameiomba mahakama kumuhoji mshtakiwa huyo akiwa gerezani.
Mahakama imeridhia mshtakiwa huyo kuhojiwa na kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 8, 2018 itakapo kuja kwa ajili ya kutajwa.
Mbali na Yusufali na Mandago washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni
Isaack Kasanga, Taherali Sujjauddin Taherali na Mohamed Seif ambapo wanakabiliwa na mashtaka 39 likiwemo la kuisababishia serikali hasara ya Sh. Bilioni mbili.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Kati ya Machi 2,2010 na Aprili 26,2016 katika maeneo tofauti ndani ya Jiji la Dar es salaam walikula njama kwa kughushi,kukwepa kulipa kodi.
Katika shitaka la utakatishaji fedha washtakiwa wanadaiwa kati ya Machi 4,2011 na 13 Aprili 2016 katika maeneo tofauti ndani ya Mkoa wa Dar es salaam akiwa mmiliki na Mkurugenzi wa kampuni ya Superior Financing Solution Limited walijihusisha na muamala wa kiasi cha shilingi (2,967,959,554) wakijua fedha hizo zinatokana na zao la pesa haramu.