Serikali ya Sudan Kusini imesisitiza dhamira yake ya kukomesha uandikishaji na utumiaji wa wanajeshi watoto.
“Wizara ya Jinsia, Watoto, na Ustawi wa Jamii inatambua uzito wa suala hili, na tuna nia ya dhati ya kukomesha uandikishaji na matumizi ya askari watoto.
“Tunafanya kazi kwa bidii na washirika wetu ili kuhakikisha kwamba watoto hawaandikishwi tena, kwamba wale ambao wameachiliwa wanasaidiwa, na kwamba sababu za msingi za kuajiri watoto zinashughulikiwa,” Esther Ikere, katibu mdogo katika Wizara ya Jinsia, Watoto na Ustawi wa Jamii, alisema katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Askari Watoto katika mji mkuu wa Juba.
Siku hiyo, inayojulikana pia kama Siku ya Mikono Nyekundu, huadhimishwa kila mwaka mnamo Februari 12.
Jenerali Ashhab Khamis Fahal, msaidizi wa mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Sudan Kusini, alisema serikali imejitolea kuwalinda watoto hao.
“Tumejipanga katika utekelezaji wa mpango kazi wa kina tuliosaini na wabia na taasisi nyingine za Serikali, na tumetekeleza wajibu wetu kwa kufikisha taarifa hizo ngazi ya chini hususani makamanda wanaosimamia vikosi hivyo ni jukumu lao kuhakikisha kuwa hakuna aina yoyote ya uajiri wa watoto kati ya vikosi hivyo. Kwa hivyo wanapaswa kuhakikisha kuwa watoto hawaandikishwi,” aliongeza.