Lori jipya lawasili katika mji wa Renk, Sudan Kusini, likiwa limejaa makumi ya wanaume wazee, wanawake na watoto, nyuso zao zilizochoka zikionyesha hali ngumu ya safari yao kutoka Sudan iliyoharibiwa na vita.
Ni miongoni mwa zaidi ya watu nusu milioni ambao wamevuka mpaka na kuingia Sudan Kusini, ambayo inatatizika kuwahudumia waliowasili wapya.
Renk iko kilomita 10 tu (maili sita) kutoka Sudan, ambako mapigano yalizuka mwezi Aprili mwaka jana kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, kamanda wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Tangu wakati huo, vituo viwili vya usafiri vya Renk vinavyosimamiwa na Umoja wa Mataifa vimezidiwa na mmiminiko wa watu wenye hofu bila kuingiliwa, wakikimbia kuokoa maisha yao.
Safari imejaa hatari, alisema Fatima Mohammed, mwalimu mwenye umri wa miaka 33 ambaye alitoroka na mumewe na watoto watano kutoka mji wa El-Obeid katikati mwa Sudan.
“Risasi zilikuwa zikiingia ndani ya nyumba yetu. Tulinaswa katikati ya mapigano katika barabara yetu wenyewe. Kwa hivyo tulielewa kwamba tulihitaji kuondoka kwa manufaa ya watoto wetu,” aliiambia AFP, akielezea hali ya Sudan kama “sio endelevu”.