Kiongozi mkuu wa Sudan ameonya Umoja wa Mataifa kwamba vita vya nchi yake vinaweza kusambaa katika mataifa jirani ya Afrika.
Katika hotuba yake, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan pia aliitaka jumuiya ya kimataifa kuwateua wapinzani wake, kundi la Rapid Support Forces (RSF), kundi la kigaidi.
Wakati huo huo, kiongozi wa RSF Hamdan Dagalo alisema yuko tayari kwa usitishaji mapigano.
Tangu Aprili, Sudan imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya maelfu ya watu.
Huko nyuma mnamo 2021, majenerali hao wawili walifanya mapinduzi, lakini katika miezi ya hivi karibuni mzozo wa kuwania madaraka kati yao umesababisha watu wao kuchukua silaha dhidi ya kila mmoja.
Akizungumza na Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi, Jenerali Burhan alisema chama chake kiko tayari kwa mazungumzo ya amani, na alitaka “kukomesha vita hivi na kupunguza mateso ya watu wetu”, lakini akasema RSF ilikataa.
Hata hivyo, katika ujumbe adimu wa video kwa Umoja wa Mataifa, mpinzani wake, Jenerali Dagalo – anayejulikana pia kama Hemedti – alisema yuko tayari kushiriki mazungumzo.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan vilizuka mwezi Aprili wakati wanachama wa RSF waliposambazwa nchini kote katika hatua ambayo jeshi, likiongozwa na Jenerali Burhan, liliona kama tishio.
Inabishaniwa ni nani aliyefyatua risasi ya kwanza lakini mapigano yaliongezeka haraka katika maeneo tofauti ya nchi. Mapigano hayo yamesababisha vifo vya takriban watu 7,500 kulingana na shirika lisilo la kiserikali la Acled na kuwakimbia mamilioni ya watu.
Jenerali Burhan, ambaye alikuwa kiongozi mkuu wa Sudan kufuatia mapinduzi ya mwaka 2021, amekuwa akizunguka dunia nzima kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa.