KAMPUNI ya SUKA ambayo inatoa huduma ya teksi mtandaoni imezinduliwa jijini Dar es Salaam na imeelezwa kujibu changamoto za madereva na kutoa huduma bora kwa abiria.
Uzinduzi huo ulifanyika jana maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Godfrey Daniel.
Alisema SUKA ni mfumo unaounganisha madereva na abiria kwa njia ya mtandao na teknologia nyingine.
“Katika lugha ya Kiswahili neno “Usukuani” ni kifaa cha kuongozea chombo cha usafiri kama gari, piki piki, meli, ndege, nk. Sasa kutokana na neno hilo kukazaliwa au kuibuka neno jingine lisilorasmi “SUKA” ikiwa ni mshika usukani au anayesuka njia yaani dereva,” alisema
Alisema tangu awali kuanzia kwenye wazo na katika shughuli zote za ujenzi na ukamilisho wa mfumo wa SUKA lengo limekuwa kuboresha na kujaribu kupunguza kama si kuondoa kero na changamoto anazopata dereva wa mtandao.
Alisema watayaarishaji wa SUKA wanaamini kuwa ikiwa dereva atakuwa mwenye furaha na mafanikio kwenye kazi yake basi hata viwango vya huduma yake vitakuwa bora zaidi na hivyo kuboresha huduma kwa mteja wake ambaye ni abiria.
“Baada ya utafiti tulioufanya tuligundua na kutafuta suluhisho la changamoto ambazo dereva amekuwa akikumbana nazo ikiwemo makato ya juu, upatikanaji wa chenji, kutoheshimika katika kazi, kutokuwa na uhakika wa ajira mtandaoni kutokana na wenye mifumo kuizima au kumfungia dereva ama mabadiliko ya bei na mengineyo bila taarifa,” alisema.
Alisema SUKA ni mfumo unaofanyakazi na pia kutumika kwenye simu janja za Android na Apple na kwamba kama ilivyo mifumo ya namna hiyo kuna App kwa ajili ya dereva na pia ya abiria.
“ Tunajua kuwa madereva wako tayari na wamekuwa wakifanya shughuli zao kama kawaida na kupitia mifumo mbali mbali iliyopo. Dhumuni la kuleta SUKA na kinachotutofautisha na mifumo mingine ni kuwa sisi dereva ndiyo mteja wetu wa kwanza hivyo tumezingatia na tutaendelea kuboresha na kushirikiana na madereva walio na nia na utayari,” alisema.
Alitaja vigezo vya kujiunga na mfumo wa SUKA na kuanza kutoa au kutumia huduma za usafiri kuwa kamaifuatavyo. Kwa Dereva (SUKA) anahitajika kuwa na Leseni ya udereva halali iliyohai, Bima ya chombo husika iliyohai, Cheti cha LATRA kilichohai, Simu janja na namba iliyosajiliwa.
Mkurugenzi huyo alisema abiria anahitaji kuwa na simu janja na namba iliyosajiliwa, Pesa au salio la kulipia usafiri. Kujiunga Dereva(Suka) – tuma vifuatavyo kwa pamoja kupitia tovuti yetu www.sukaride.com, picha ya dereva inayoonyesha sura, picha ya leseni inayoonyesha maelezo yote, picha ya chombo inayoonyesha plate number vizuri, anwani yako ya barua pepe na namba yako ya simu janja.
“Abiria anapaswa kupakua app ya SUKA (ya blue kwa abiria) toka google play (android) au app store (iphone) tovuti yetu ya sukaride.com,” alisema Mkurugenzi