Rais wa Chad Idriss Deby amefariki Dunia baada ya kupata majeraha kwenye mapambano dhidi ya Waasi, Deby amefariki ikiwa imepita siku moja tangu atangazwe kushinda Uchaguzi wa Urais wa Nchi hiyo kwa muhula wa sita.
Jeshi la Chad limesema Rais huyo kabla ya kifo chake aliungana na Wanajeshi ambao walikuwa mstari wa mbele kupambana na Waasi ambao walifanya mashambulizi wakijaribu kuuteka Mji Mkuu (N’Djamena) na huko ndiko alipopata majeraha, bado taarifa zaidi hazijatolewa.
Rais Deby alitangazwa na Tume ya Uchaguzi jana jioni kuwa Mshindi wa Urais kwa muhula wake wa sita madarakani, Deby ameliongoza Taifa hilo la Afrika ya Kati kwa zaidi ya miongo mitatu.
Alitangazwa Mshindi kwa 79% ya kura, licha ya Wapinzani wake Wakuu kuamua kususia uchaguzi huo wa Aprili 11, Waziri Mkuu wa Zamani, Albert Pahimi Padacke ameshika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro hicho kwa kupata 10.32% na idadi ya waliojitokeza ilikuwa 64.81%.