Kama inavyofahamika, bei ya mafuta ghafi duniani imeendelea kupanda kwa kasi na kwa kiwango kikubwa, kutoka dola 50 kwa pipa mwezi wa Januari mwaka huu hadi dola 86 kwa pipa.
Leo tarehe 31 Oktoba 2021 hali hii inapelekea bei kupanda kwenye vituo vya kuuzia mafuta na mitaani hapa nchini.
Kama itakavyokumbukwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alielekeza hatua mbalimbali za kikodi, kisheria/kanuni na kiutawala ili kupunguza makali na athari za ongezeko hili la bei. Wizara ya Nishati imeanza kutekeleza maelekezo hayo na pia kuratibu hatua mbalimbali za Wizara na taasisi nyingine za umma na kufanikiwa kupunguza ongezeko kubwa la bei ya mafuta kwa mwezi wa Oktoba.
Katika kutimiza azma ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba bei za mafuta haziumizi wananchi, na shughuli za uchumi haziathiriki, Wizara ya Nishati ilichunguza na kubaini uwezekano wa unafuu wa bei iwapo Serikali yenyewe itanunua mafuta moja kwa moja kutoka kwenye mitambo ya kusafisha mafuta (refineries) ya nchi rafiki badala ya kuachia watu wa katikati (intermediaries) kununua kwa nchi hizo hizo rafiki zetu na kutuuzia kwa bei kubwa.
Kutokana na hilo, katika duru la kwanza, kuanzia tarehe 22 hadi 29 Oktoba 2021 nilifanya ziara katika nchi tatu – Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Algeria – ambazo zinazalisha mafuta kwa wingi na kuuza kote duniani. Katika nchi hizo, nilikutana na Mawaziri wenzangu wa Nishati, na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na makampuni 2 ya mafuta ya Serikali za nchi hizo. Vilevile, nilibeba ujumbe maalum wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa viongozi wa nchi hizo.
Katika ziara hiyo, niliongozana na Ndugu Michael Mjinja, Kamishna wa Petroli na Gesi katika Wizara ya Nishati na Ndugu James Mataragio, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC. Pia, mabalozi wetu katika nchi hizo walishiriki katika vikao na mazungumzo niliyoyafanya.
MAKAMBA ATINGA TANESCO ATOA MAAGIZO MAZITO “TUTAWAONDOA KATIKA NAFASI ZENU”