Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation kwa kushirikiana na Benki ya NBC imewafadhili wanafunzi 50 wa Chuo cha Afya ya Sayansi Cha Morogoro (Morogoro College of Health and Allied Sciences) wa kada ya Ukunga ambao wapo kwenye ajira ili kuongeza ujuzi katika utendaji kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kusaini mikataba hiyo kati ya BMF, serikali na chuo hicho, Afisa Mtendaji Mkuu Benjamin Mkapa Foundation Dr. Elleni Mkondya amesema, wauguzi wanaonufaika na ufadhilii huu ni wale waliopo kwenye ajira rasmi ili kuwaendeleza kimasomo kupunguza changamoto ya vifo vya mama na mtoto.
Dr. Ellen amesema wanafunzi hao watasoma kwa muda wa mwaka mmoja ngazi ya diploma huku malengo ya BMF ni kuzunguka Nchi nzima, ambapo wakunga 50 wengine kutoka Mkoa wa Mwanza watakuwa ni wanufaika wa Pili kwa ufadhili huo wa masomo, idadi ambayo itafikisha wakunga 100 kwa Mikoa ya Morogoro na Mwanza.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Benki ya NBC Godwin Semunyu, amesema shauku yake ni kuona idadi ya vifo vya mama na mtoto vinapungua nchini wakati wa kujifungua.
Amesema ufadhili huo umelenga kukuza ujuzi kwa wakunga hao ili kuongeza tija kwa Taifa, na ni sehemu ya matokeo ya NBC Dodoma Marathoni iliyofanyika Mwezi Julai 2023 ambapo kwa kipindi cha miaka miwili benki itafadhili kiasi cha shilingi milioni 211.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa Morogoro Dokta Kusirye Ukio akimwakilisha katibu Tawala Mkoa Morogoro Dokta Mussa Ally Mussa, amesema licha ya serikali kutoa vifaa tiba mara kwa mara, bado kuna changamoto ya vifo kwa wajawazito katika vituo vya huduma ya afya, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kupunguza adha hiyo.
Anasema mpango wa Serikali ni kuendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wote wa kada ya Afya (Wakunga) kwani tayari mafunzo hayo yamezaa matunda baadhi ya maeneo hasa vijijini.