Wananchi wa Hanang wanaendelea kuishukuru Serikali pamoja na Wadau mbalimbali wanaoendelea kuwa sehemu ya faraja kwa waathirika wa Mafuriko wilayani humo ambapo leo Benki ya Stanbic Bank Tanzania imetoa msaada wa vyakula vyenye thamani ya shilingi Milioni kumi kuwasaidia waathirika wa maporomoko ya tope, mawe na magogo katika Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara.
Mkurugenzi Kitengo cha wateja binafsi StanBank Tanzania Omari Mtiga amesema wametoa msaada huo kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan aliechukua hatua za haraka kuwasaidia wananchi waliokumbwa na Maafa hayo alfajiri ya Desemba 3,2023 na kusababisha vifo 89 na wengine kujeruhiwa Vibaya.
Ameitaja misaada waliyoitoa ni mchele,unga, maharage na Mafuta ambavyo vyote thamani yake ni shilingi Milioni 10.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Hanang’ Francis Namaumbo ameishukuru benki hiyo kwa kutoa msaada huo na kwamba serikali itasimamia kikamilifu ili misaada hiyo iwafikie walengwa.
Aidha Viongozi hao wa Stanbic bank walitembelea maeneo yaliyoathiriwa zaidi na maporomoko hayo katika mji wa Kateshi kushuhudia hali ilivyokuwa nakuzungumza na wathirika wa Mafuriko hayo wakiwemo Wafanyabiashara.