Taasisi ya Taawanu Islamic Foundation chini ya Mkurugenzi wake wa Kimataifa Hajat Zahra Dattan imetoa mafunzo ya Ujasiliamali kwa akina mama Mkoa wa Kagera wakiwakilishwa na wanawake watatu watatu kutoka kila Wilaya lengo ikiwa ni kuongeza ujuzi wa mambo mbalimbali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Mafunzo hayo yametolewa katika msikiti wa Bilele uliopo Manispaa ya Bukoba,huku washiriki hao na wasindikizaji wao kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera wakishuhudia na kufundishwa namna bora ya kutengeza sabuni,viungo vya chai,unga wa lishe ikiwa ni sambamba na kupewa elimu juu ya mwanamke wa kiislamu na uchumi,umuhimu wa kuisoma dini ya kiislamu na mambo mengine mbalimbali.
Mafunzo hayo yaliyoendeshwa na wataalamu kutoka taasisi ya TAAWANU Naifath Wilbroad na Sauda Amiri wakiongozwa na mwenyekiti wa wao Wilaya ya Bukoba Mwl Juma Said,pia yamehudhuriwa na Mkurugenzi wa Taawanu Kimataifa Hajat Zahra Dattan,Mwenyekiti wa Taawanu Taifa Sheikh Hashim Kamgunda wakiwa na Sheikh wa Mkoa wa Kagera Sheikh Haruna Kichwabuta ambao wamewahimiza washiriki wa mafunzo hayo kufanyia kazi kile walichofundishwa na kuwafundisha wengine waliowaacha kwenye maeneo yao ili mwisho wa siku elimu hiyo iwafikie walio wengi na waweze kujikwamua kiuchumi kupitia ujasiliamali.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Taasisi ya TAAWANU kwa kuwafikia na kuamua kuwaonyesha njia ya kujikwamua kimaisha kupitia ujasiliamali huku wakiahidi kuyafanyia kazi waliyojifunza na kuwanufaisha wengine waliowaacha kwenye maeneo yao.