Chama cha wakala wa forodha Tanzania (TACAS) kimeiomba Serikali kuwapatia fursa mbalimbali za bandari kwani wanaweza kuongeza ubunifu katika utendaji kazi hasa kusaidia ukusanyaji mapato na kuwezesha wafanyabiashara kupata huduma bora na kwa wakati.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chama cha wakala wa forodha Tanzania Ephraim Mwankusiye, wakati wa kikao kazi baada ya kumaliza uzinduzi wa chama hicho.
“Tunatambua mchango kwa wadau mbalimbali wa sekta ya bahari lakini tuwaombea Serikali huu ni wakati mzuri tumeona tunaweza kwenda na kasi kubwa ambayo serikali ya awamu ya sita inakwenda nayo, Bandari yetu ya Dar es Salaam ni kubwa Afrika Mashariki huu ni wakati wa kuongeza namba za mapato ya nchi pamoja na Ukanda wetu”. Amesema Mwankusiye.
Hata hivyo naye Katibu mtendaji wa Chama cha Wakala wa Forodha Tanzania Aloyce Kavuma, amesisitiza kuwa “Tunakwenda kutengeneza daraja la mawasiliano lenye kasi na tija kwa lengo la kupunguza gharama zinazoongezeka za mizigo bandarini, wadau wa maendeleo na wafanyabiashara tunawaomba mkipokea vizuri chama cha wakala wa Forodha nchini”.