Waziri wa Kilimo Hussein Bashe leo ametoa hotuba kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara hiyo kwa mwaka 2023/2024 Bungeni Dodoma ambapo amesema Kwa kuzingatia takwimu za uzalishaji na mahitaji ya chakula, kwa mwaka 2022/2023 Taifa limejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 114.
Bashe amesema “Tathmini ya mwisho ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa mwaka 2021/2022 imebaini kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula umefikia tani 17,148,290 kwa mlinganisho wa nafaka (Grain equivalent) ikilinganishwa na tani 18,665,217 mwaka 2020/2021 ikiwa ni pungufu ya tani 1,516,927.
“Upungufu huo umetokana na mtawanyiko wa mvua usioridhisha, kati ya kiasi kilichozalishwa, nafaka ni tani 9,233,298 na mazao yasiyo nafaka ni tani 7,914,992, aidha uzalishaji wa nafaka ambao unahusisha mahindi, mchele, mtama, uwele, ulezi na ngano ulipungua kwa tani 1,641,127 sawa na asilimia 15.1 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani 10,874,425 kwa msimu wa 2020/2021”
“Uzalishaji wa mazao yasiyo nafaka ambayo ni jamii ya mikunde, muhogo, ndizi, viazi vitamu na mviringo uliongezeka kwa tani 124,200 sawa na ongezeko la asilimia 1.6 na kufikia tani 7,914,992 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani 7,990,792 msimu wa 2020/2021, mahitaji ya chakula kwa mwaka 2022/2023 ni tani 15,053,299 na ziada ni tani 2,095,256 za chakula”
“Kwa kuzingatia takwimu hizo za uzalishaji na mahitaji ya chakula, kwa mwaka 2022/2023 Taifa limejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 114”