Mahakama moja mjini Taipei imewafunga jela wanajeshi wanane wa Taiwan kwa kufanya ujasusi kwa niaba ya China ili wapate pesa.
Maafisa wa kijeshi waliostaafu waliwahonga askari waliokuwa kazini dola 21,900 za Kimarekani ili wajiunge na mtandao wa kijasusi, mahakama ilibaini.
Mmoja wa watu hao, ambaye aliaminika kuwa muhimu katika kuwasajili wanajeshi, alihukumiwa kifungo cha miaka 13 gerezani.
Mmoja wa wanajeshi hao, Luteni Kanali, alihukumiwa kifungo cha miaka tisa kwa kupanga kuhamia China kwa kuruka kutoka kwenye helikopta, huku mwingine akipiga video ya mafundisho kuhusu kujisalimisha kwa China katika tukio la vita.
China inaichukulia Taiwan inayojitawala kama jimbo lake lililojitenga na ambalo hatimaye litakuwa chini ya udhibiti wake, imekuwa ikifanya kila juhudi kuchukua kisiwa hicho.
Pande hizo mbili zimekuwa zikifanya ujasusi tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya China mwaka 1949.