Takriban watu 13 wamekufa mashariki mwa Uganda baada ya maporomoko ya ardhi kuzika nyumba 40 katika vijiji sita, maafisa wa kutoa misaada walisema Alhamisi.
Chama cha Msalaba Mwekundu cha Uganda kimesema miili 13 imeopolewa na juhudi za uokoaji zinaendelea.
Vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti kwamba viongozi wanatarajia idadi ya vifo inaweza kuongezeka hadi 30.
Maporomoko hayo yametokea baada ya mvua kubwa kunyesha usiku wa kuamkia leo katika wilaya ya milimani ya Bulambuli, ambapo maporomoko ya ardhi ni ya kawaida. Wilaya hiyo iko takriban kilomita 280 (maili 173) mashariki mwa mji mkuu, Kampala.
Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda John Cliff Wamala amesema miili 13 imepatikana. Amesema zaidi ya nyumba 40 zimeharibiwa kabisa. Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uganda ilitoa tahadhari, ikiandika kwenye mtandao wa X kuwa mvua kubwa iliyonyesha jana Jumatano katika maeneo tofauti ya Uganda ilisababisha maafa katika maeneo mengi.
Taifa hilo la Afrika Mashariki limekumbwa na mvua kubwa katika siku za karibuni, huku kukishuhudiwa mafuriko kaskazini magharibi mwa nchi baada ya mkondo wa Mto Nile kuvunja kingo zake.