Makumi ya watoto walikufa maji walipokuwa wakioga kwenye mito na madimbwi katika ibada [matambiko] ambayo ilikuwa sehemu ya tamasha la siku tatu la Wahindu katika jimbo la Bihar mashariki mwa India, maafisa walisema.
Mvua kubwa za masika hivi majuzi ziliongeza viwango vya njia za maji katika jimbo lote.
Takriban watu 46, wakiwemo watoto 37, walikufa maji katika matukio tofauti katika wilaya 15 za jimbo hilo, taarifa kutoka idara ya usimamizi wa maafa ya Bihar ilisema. Mamlaka imepata miili 43 kufikia sasa, na watu watatu waliotoweka wanakisiwa kuwa wamekufa.
Wakati wa tamasha la kila mwaka, akina mama hufunga kwa saa 24 kwa ajili ya ustawi wa watoto wao. Wakati fulani wanawake hao huambatana na watoto wao wanapotembelea mito na madimbwi kwa ajili ya ibada za utakaso. Tamasha hilo lilihitimishwa Alhamisi.
Serikali ya jimbo hilo imetangaza fidia ya rupia 400,000 ($4,784) kwa familia za kila mmoja wa waliofariki.
Ajali mbaya kama vile kuzama na kukanyagana wakati wa sherehe za kidini ni za kawaida nchini India.