Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa mashambulizi yanayohusiana na kundi la waasi wa M23 yamesababisha vifo vya takriban watu 3,000 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mapigano hayo yamesababisha majeruhi wengi na kusababisha zaidi ya watu 700,000 kuyakimbia makazi yao huku hali ya kibinadamu ikizidi kuwa mbaya
Licha ya tangazo la usitishaji mapigano, mapigano bado yanaendelea katika baadhi ya maeneo, hali inayoongeza hofu miongoni mwa wakazi wa Goma na vitongoji vyake. Serikali ya DRC imeendelea kusisitiza kuwa itaendelea kupambana na waasi hao ili kurejesha utulivu katika eneo hilo
Mashirika ya misaada yameripoti kuwa hospitali zimezidiwa uwezo kutokana na idadi kubwa ya majeruhi na wahanga wa mapigano. Vyumba vya kuhifadhia maiti pia vimejaa, na kuna uhaba mkubwa wa dawa na vifaa tiba vinavyohitajika kwa matibabu ya dharura
Katika hatua nyingine, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imeeleza kuwa inafuatilia kwa karibu hali inayoendelea, huku uchunguzi ukiendelea kuhusu madai ya uhalifu wa kivita uliofanyika katika jimbo la Kivu Kaskazini tangu Januari 2022