Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya imesema itafuatilia mchakato mzima wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, ili kudhibiti vitendo vya rushwa na kuhakikisha wanapatikana viongozi wanaostahili.
Aidha, imeviomba vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla kutoa taarifa pale watakapoona viashiria vya rushwa kwenye maeneo yao ili vidhibitiwe mapema kabla havijasababisha madhara kwenye mchakato huo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Maghela Ndimbo alisema hayo kwenye kikao na viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kilicholenga kufanya tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mikakati ya uchaguzi mkuu ujao.
Ndimbo alisema katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, taasisi hiyo haikupokea kesi yoyote ya rushwa wala taarifa za vitendo hivyo kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo na hivyo wanajipanga zaidi kudhibiti vitendo hivyo uchaguzi ujao.
“Pamoja na kampeni yetu ya ‘Takukuru rafiki’, tunahitaji ushirikiano wa pamoja na wadau ikiwamo vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla ili tuweze kufikia malengo yetu ya kutokomeza vitendo vya rushwa,” alisema Ndimbo.
Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale alisema ili kumaliza vitendo vya rushwa TAKUKURU inapaswa kuendelea kutoa elimu juu ya haki pamoja na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa kwa wanaobainika kujihusisha na vitendi hivyo.
Alisema rushwa imekuwa ikisababisha haki za watu kupotelea mikononi mwa wasiostahili haki hiyo na hivyo kusababisha demokrasia kuharibika ndani ya nchi.