Kundi la Taliban nchini Afghanistan limetangaza siku tatu za kusitisha vita kote nchini humo kwa ajili ya kutowa nafasi ya sherehe za kumalizika mfungo wa Ramadhani za Eid-al-Fitr.
Tangazo la Taliban limetolewa ikiwa ni siku mbili baada ya kundi hilo kulaumiwa kwa mauaji ya zaidi ya watu 50 wengi wakiwa ni wasichana wadogo, katika shambulizi la bomu lililofanywa nje ya shule moja katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul.
Wizara ya mambo ya ndani ya Afghanistan imeripoti leo Jumatatu kwamba kiasi watu 11 wameuwawa katika matukio tofauti saa chache kabla ya tangazo la Taliban la kusitisha ghasia.
Vifo hivyo vimetokana na mlipuko wa bomu dhidi ya basi katika Mkoa wa Zabul. Kadhalika tangazo la Taliban limekuja wakati ambapo Marekani inaendelea kuondowa wanajeshi wake 2,500 wa mwisho katika nchi hiyo.