Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema Tamasha la Kilimanjaro Cultural Festival linalohusisha utamaduni wa vyakula ,ngoma na lugha za asili za jamii ya Wachaga, Wapare na Wamaasai litasaidia kukuza utalii wa Mkoani Kilimanjaro endapo litaendelezwa na kutumika ipasavyo.
Amesema lengo la Tamasha hilo ni kukuza na kuhamasisha utalii wa malikale ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro sambamba na kuenzi mila na desturi za jamii za Mkoa huo zinazojumuisha Wapare, Wachaga na Wamaasai.
Ameyasema hayo leo Desemba 28,2023 alipokuwa akifunga tamasha hilo lililofanyika katika viwanja vya Kili Home Garden, Moshi Mjini Mkoani Kilimanjaro.
“Nimeshuhudia vyakula vya kiasili vya jamii za Mkoa wa Kilimanjaro vilivyoandaliwa kwa ustadi mkubwa, tukio hili limenikumbusha masuala ya afya kuhusu umuhimu wa vyakula vya asili ikiwa ni pamoja na kukinga miili yetu na kujenga nguvu mwilini na hii ndiyo sababu zamani Wazee wetu waliishi miaka mingi bila ya kusumbuliwa na maradhi ya mara kwa mara.” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Pia, amesema ameshuhudia ngoma za asili za kipare, kimaasai na kichaga, lugha za asili za Kipare, Kimaasai na Kichaga ambazo zinawakumbusha vijana kuenzi mila na tamaduni zao ili waweze kufahamu walikotoka na wanakoelekea.
“Natoa wito kwa vikundi vya ngoma kuendelea kukutana kila wakati na kubadilishana uzoefu baina ya kikundi kimoja na kingine kwa sababu ngoma za asili ni kivutio kikubwa kwa watalii wanaokuja kutembelea vivutio vyetu nchini Tanzania” Mhe. Kairuki amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki amezindua program ya ‘’Kilimanjaro Home Stay’’ inayohusu utaratibu wa kutumia nyumba za wenyeji kutoa huduma za malazi kwa wageni hususan kipindi cha matukio makubwa kama vile mbio za Kilimanjaro Marathoni ili kukuza vipato kwa jamii moja kwa moja.