Leo April 14,2023 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki ameliomba Bunge likubali kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kiasi cha Shilingi Trilioni Tisa Bilioni Mia Moja Arobaini na Nne Milioni Ishirini na Moja na Mia Sita Tisini na Tisa Elfu (Tsh. 9,144,021,699,000).
Kwa upande wa Sekta ya Elimu ya Msingi na Sekondari Waziri Kairuki ametaja maendeleo yaliyopewa kipaumbele ikiwemo kugharamia elimu bila ada kwa Shule za Msingi na Sekondari ambapo Shilingi Bilioni 399.64 zimetengwa.
“Kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 157.79 zimetengwa kwa ajili ya Shule za Msingi na Shilingi Bilioni 241.85 zimetengwa kwa ajili ya Shule za Sekondari”
“Bajeti hiyo ni sawa na ongezeko la Shilingi Bilioni 53.15 sawa na asilimia 15.34 ikilinganishwa na bajeti ya Shilingi Bilioni 346.49 iliyoidhinishwa katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23, ongezeko hili linatokana na Wanafunzi wa kidato cha tano na sita kujumuishwa katika Mpango wa Elimu Bila Ada”