Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) lina mpango wa kujenga kituo kidogo cha umeme (Switching Station) kwenye Wilaya ya Ushetu eneo la Nyamirangano ili kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme wilayani humo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akijibu swali la Mbunge wa Ushetu Mhe. Emanuel Peter Cherehani aliyetaka kujua je nini mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme wa uhakika katika halmashauri za Ushetu, Msalala, na Kahama.
Aidha, Mhe. Kapinga amesema sambamba na hilo TANESCO pia itaongeza njia nyingine za umeme kutokea kituo hicho kwenda Ushetu, Msalala, na Kahama ili kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme.
Amesema, ujenzi wa mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 12 na mradi unategemewa kukamilika Mwaka wa Fedha 2024/2025.