Tanzania na Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa (UN Tourism) zimesaini mkataba wa makubaliano utakaoifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano la Pili la Kikanda la Utalii wa Vyakula la Shirika la Umoja wa Mataifa (The 2nd UN Tourism Regional Forum on Gastronomy Tourism for Africa) linalotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Machi 11 hadi 13, 2025.
Hafla ya utiaji saini imefanyika kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa jijini Madrid, Hispania leo Januari 24,2025.
Akizungumza katika hafla hiyo, Chana amesema Tanzania inafuraha kuwa mwenyeji wa kongamano hilo linalotarajia kukutanisha washiriki zaidi ya 300 kutoka mataifa mbalimbali duniani na kwamba kupitia kongamano hilo Tanzania itajifunza kutoka mataifa hayo namna wanavyofanya katika kukuza utalii wa vyakula.
“Kupitia Kongamano hili tunataka kuwajengea uwezo wapishi wetu jinsi ya kutengeneza aina tofauti za vyakula ili watalii wanapokuja waweze kufurahia vyakula vya nyumbani kwao lakini pia tunahitaji kuona ni fursa gani zitakazotokana na kongamano hilo ili tuweze kujifunza utangazaji utalii wa vyakula” Chana amesisitiza.