Tanzania imeteuliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 73 wa Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege (Airports Council Interantional-ACI) kwa Kanda ya Afrika,huku maandalizi yake yakiendelea vizuri.
Ameyasema hayo leo,Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa wakati akiongea na waandishi wa habari katika uwanja wa Ndege Kisongo Jijini Arusha juu ya Mkutano wa Kikanda 73 wa Baraza la Viwanja vya Ndege Afrika na maonesho ya wadau utakaofanyika Aprili 24 hadi 30 mwaka huu jijini humo.
Amesema mkutano huo umepangwa kufanyika siku saba jijini hapo na kuwaleta wajumbe wasiopungua 400 nchini.”Mkutano huu utaanza na Mkutano Mkuu, Mikutano ya Bodi na Mikutano ya Kamati mbalimbali za Kitaalam huku zikiambatana na shughuli mbalimbali,”amesema.
Amesema miongoni mwa shughuli nyingine zitakazofanywa na wageni hao ni kutembelea vivutio mbalimbali vya kitalii ambapo katika siku saba za mkutano huo, imetengwa siku moja ambapo takriban wageni 300 watatembelea mbuga ya wanyama ya Bonde la Ngorongoro na wengine watatembelea vituo mbalimbali vya kitalii hapa Jijini Arusha.
Amesema kaulimbiu ya mkutano huo ni “Katika kuelekea Wakati Ujao Bora wa Kijani: Kutumia Usafiri wa Anga Endelevu na Utalii kwa Ustawi wa Kiuchumi”ambapo ni tukio litakaloangazia umuhimu wa kuzingatia maendeleo endelevu katika usafiri wa anga na kuonyesha dhamira ya Tanzania katika utunzaji wa mazingira.
“Mkutano huo utakuwa na faida mbalimbali kwa nchi ikiwa ni pamoja na kuwaongezea ujuzi wazawa katika masuala ya usafiri wa anga na utalii kupitia kujifunza mbinu bora za kimataifa zinazotumika katika kuboresha sekta hizo.
“Pia litatoa fursa kwa wazawa kujifunza kuhusu utoaji wa huduma bora na ufanisi wa utendaji kazi katika sekta hizo na kufanya wazawa kunufaika kupitia makampuni yao kushiriki moja kwa moja katika kutoa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za mahoteli, huduma za vyakula, huduma za usafiri, huduma za kitalii na biashara pamoja na kuongeza ajira katika mahoteli, Kampuni za Utalii na Wajasiliamali kwa lengo la kuongeza fedha za kigeni na ongezeko la kodi.
“Pia itakuwa fursa ya kutangazwa kwa vituo vya kitalii, viwanja vya ndege vya Kimataifa vya Tanzania kupitia matangazo mubashara na mitandao mbalimbali ya kijamii na vituo vya televisheni vitakavyorusha mkutano huo,”amesema.
Amesisitiza kuwa serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuweka mazingira rafiki ya kuifanya nchi kuwa sehemu ya utalii wa mikutano mikubwa ya Kimataifa Barani Afrika.
Kwa upande wake Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Abdul Mombokaleo amesema TAA inaendelea na kasi za mabadiliko yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo menejiment imejipanga kuwekea vipaumbele vya msingi kuhakikisha vinaboresha utendaji kazi na huduma ya viwanja vya ndege.
Amesema kuwa mkutano huo ni mkubwa unahusisha wadau wa viwanja vya ndege wa nchi za afrika kwani sekta hiyo ni sekta mtambuka ambapo ndani ya viwanja vya ndege kuna wadau wengi wanashiriki kibiashara.
“Tunaamini mkutano huu unapofanyika nchini ni fursa ya kipekee kuweza kujitangaza na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara hivyo ni nafasi kubwa kwa Tanzania kujitangaza,”amesema
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Paul Makonda , ameshukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wizara hiyo kwa Kuiteua Arusha kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa, akiahidi usalama wa kutosha pamoja na huduma nzuri kwenye maeneo ya malazi na kumbi za mikutano kwa wageni wote kwa siku zote saba za kufanyika Mkutano huo.
Makonda amesema mkutano huo utakuwa sehemu nyingine ya kusisimua uchumi wa Mkoa wa Arusha kupitia sekta ya Utalii na sekta nyingine mtambuka za vyakula, usafiri, sehemu za starehe, hoteli na nyumba za kulala wageni.