Michezo

Tanzania yaiadhibu Uganda Copa Cocacola Kenya

on

Jumanne ya December 03, 2019 timu ya mpira wa miguu ya COPA Coca-Cola ya Tanzania ya vijana chini ya umri wa miaka 16 imeendelea kufanya vizuri katika mashindano ya COPA Coca-Cola Afrika yanayofanyika mjini Thika nchini Kenya.

Katika mchezo wa awali wa mashindano hayo, Tanzania ilichuana na Timu ya mpira wa miguu ya Afrika Kusini na kuibuka na ushindi wa goli 3-1 na baadae kucheza mchezo wa pili dhidi ya Zambia ambapo matokeo yaliisha kwa Zambia kuibuka na ushindi wa 2-0.

Michezo hiyo ambayo ni mikubwa barani Afrika inazihusisha timu 10 za barani Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya ambao ndio wenyeji wa michuano, Zambia, Afrika Kusini, Zimbabwe, Uganda, Ethiopia, Namibia, Angola, Botswana na Msumbiji.

Hata hivyo katika michuano ya robo fainali ya leo Tanzania imeikabili Uganda na kuibuka na ushindi wa goli 6-2. Safu ya ushambuliaji iliongozwa na wanafunzi na Paul Nyerere ambaye aliibuka nyota wa mchezo baada ya kufunga goli 3 peke yake. Wachezaji wengine ni Frank Zephania aliyefunga goli moja na Kassim Ibrahim aliyefunga goli moja.

Mashambulizi ya timu ya Tanzania yalikuwa ni yale ya kushitukiza lakini wakatumia muda mwingi kujilinda kwa mipango dhidi ya Uganda ambao wachezaji wake walionekana kuwa hatari kutokana na ushindi wa goli 11 kwa 1 dhidi ya Namibia siku ya ufunguzi wa michuano yaani 02.12.2019.

Abel Mtweve, Kocha wa Timu hiyo ya vijana wa chini ya miaka 16 kutoka Tanzania amepokea sifa kede kede kutoka kwa watazamaji kwa kuwa na mbinu nzuri za kusaka ushindi.

Kiongozi wa msafara ambaye pia ni makamu wa Rais UMISSETA, Mwalimu Vitalis Shija “Leo vijana hawa wamenishangaza kwa kuwa sikutarajia kabisa kuifunga timu ya Uganda goli 6, kwa kweli wameonyesha juhudi na kufuata maelekezo ya mwalimu.” Kama Serikali tupo pamoja na vijana kuwapa moyo kuwa wanaweza na natarajia mchezo wa kesho dhidi ya Kenya tutaibuka na ushindi na hatimaye kutinga fainali”.

Soma na hizi

Tupia Comments