Tanzania imeshika nafasi ya Nne kwa uzuri wa asili na kuingia katika kundi la nchi 10 zilizotajwa kwa uzuri zaidi wa asili duniani.
Kwa mujibu ripoti ya dunia kuhusu Uzuri wa Asili (Natural Beauty Report) iliyotolewa na Tovuti ya Uingereza ya Money.co.uk ambayo iliyokusanya takwimu na taarifa za wasafiri imeiorodhesha Tanzania kushika nafasi hiyo kwa kupata alama 6.98 kati ya kumi.
Vipengele vilivyoifanya Tanzania ishike nafasi ya nne ni pamoja na kuwa na mandhari nzuri za asili ikiwemo milima mashuhuri ya volcano ukiwemo Kilimanjaro ambao ni Mlima mrefu zaidi Afrika, Mlima Meru na Oldoinyo Lengai pamoja na Misitu Asilia mingi.
Pia eneo la Kreta ya Ngorongoro lenye utajiri mkubwa wa asili, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti yenye uwanda mpana na bora zaidi duniani iliyojaa Wanyamapori wakubwa na wadogo wa kuvutia, spishi mbalimbali za ndege na mimea ni sababu zilizoiwezesha Tanzania kuingia kwenye kumi bora duniani.
Sababu nyingine ni uwepo wa eneo lenye miamba ya matumbawe lenye kilomita za mraba 3,580 na uwepo wa maeneo mengi yaliyohifadhiwa yenye jumla ya Kilometa za mraba 307,873.
Katika mashindano hayo, Indonesia imetwaa taji la nafasi ya kwanza kwa kupata alama 7.77, ikifuatiwa na New Zealand 7.27, Colombia 7.16, Tanzania 6.98, Mexico 6.96, Kenya ikishika nafasi ya 6 kwa kupata alama 6.7. Nchi nyingine ni India nafasi ya saba, Ufaransa nafasi ya nane, Papua New Guinea ya tisa huku Comoro ikishika nafasi ya 10.