Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia vituo vya utafiti vya Ilonga (Morogoro) na Ukiriguru (Mwanza), kwa kushirikiana na Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imetoa mafunzo kwa wakulima wazalishaji wa mbegu za mtama 35 kutoka Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Tabora, Simiyu na Mara; juu ya mbinu, kanuni na sheria za kuzalisha mbegu za mtama, na masoko.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku tatu kuanzia Oktoba 7-9, 2024 katika kituo cha utafiti cha Ukiriguru ikiwa ni utekelezaji wa miradi ya ACCELERATED na AVISA inayotekelezwa na TARI kwa kushirikiana na taasisi za CIMMYT, CIAT na TOSCI.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo Mratibu wa programu ya utafiti wa mtama kitaifa Ndg Emmanuel Thomas Mwenda amesema lengo la mradi ni kuongeza mapokeo ya mbegu bora za mtama zilizotafitiwa na zenye tija kubwa ikilinganishwa na mbegu ambazo zimekuwa zikitumiwa na wakulima wengi.
“Katika kuhakikisha kwamba tunazitangaza mbegu bora ili ziweze kujulikana na wadau, ni muhimu kuzalisha mbegu za kutosha ili kukidhi mahitaji ya mbegu ambayo yanajitokeza.” Amesema Ndg Mwenda ambaye pia ni mtafiti kutoka kituo cha utafiti cha Ilonga chenye jukumu la kutafiti zao la mtama kitaifa.
Amesema kwa sasa kuna uhitaji mkubwa wa mbegu za mtama katika mikoa ya kanda ya ziwa na magharibi; na kwamba mafunzo hayo yatakuwa ni jawabu la changamoto ya upatikaji wa mbegu, na hatimaye kusaidia wakulima katika kuzalisha zao la mtama kwa tija.
Naye Mkaguzi kutoka TOSCI kanda ya ziwa Ndg. Evance Kaganda amesema mbali na mafunzo kuhusu kutambua sheria, kanuni na taratibu za kuzalisha mbegu bora, taasisi itaendelea kukagua mashamba ya wakulima hao ili kuhakikisha kanuni hizo zinazingatiwa.
“Watakapokuwa wameanza uzalishaji ni lazima wasajili mashamba yao, na sisi tutawajibika kwenda kuyakagua mara mbili mpaka tatu ili kuona ubora wa mbegu hizo kama unazingatiwa, na baada ya kuwa wamevuna tutawajibika kwenda na kuchukua sampuli kisha kuja kuzipima katika maabara zetu za TOSCI na kuwapa matokeo ya ubora wa mbegu zao” Amesema.
Baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo wamesema mafunzo yamewaonesha fursa nyingine katika kilimo hususani biashara ya mbegu na kwamba yote waliyojifunza watakwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo.
“Ni kama wengi tulikuwa gizani, mambo mengi tulikuwa hatuyafahamu, kwakweli tunashukuru kwa mafunzo haya na naamini tutafanya vizuri katika kilimo” Amesema Victoria Polika Mkulima mzalisha mbegu kutoka Kaliua, Tabora.
“Nilikuwa nalima kwa mazoea, lakini sasa nimejifunza namna nzuri ya kuzalisha mbegu na soko la mbegu ni la uhakika, kwahiyo kwangu hiyo ni fursa”
Amesema Bi Juliana Ngassa Mkulima wa mtama kata ya Uchunga Wilayani Kishapu.
“Nimejifunza kutumia mbegu bora za muda mfupi ambazo zinaweza kuvumilia mabadiliko ya hali ya tabia nchi ili kupata mavuno ya kutosha” Amesema Sitta Kulwa mkulima kutoka Wilayani Uyui.