Mpango kunusu kaya maskini nchini (TASAF) umetumia zaidi ya Shilingi bilioni 59 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na fedha kwa ajili ya walengwa wa mpango huo kwa kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2025 Mkoani Geita.
Fedha hizo zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu,afya,ujenzi wa barabara,utunzaji wa mazingira na ujenzi wa malambo lengo likiwa ni kuwasogezea wananchi huduma karibu na kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati ya uongozi Tasaf makao makuu waliofika mkoani Geita kwa ajili ya kukagua miradi inayotekelezwa kwa fedha za Tasaf,Katibu Tawala Mkoa wa Geita Mohamed Gombati amesema uwepo wa mpango umewezesha watoto wa walengwa wanaosoma shule za msingi na sekondari kumudu kupata mahitaji ya shule na kuendelea na masomo.
Pia amesema mpango huo umesaidia kuongeza mahudhurio ya kliniki kwa watoto chini ya miaka mitano na wazazi kupata mafunzo na malezi ya watoto,huku baadhi ya walengwa wakifanikiwa kuanzisha biashara ndogondogo kwa ajili ya kupata kipato na kuimarisha uchumi wa kaya.
Katika ziara hiyo ya siku moja Wajumbe hao wa kamati ya Uongozi Tasaf makao makuu wametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Nyabilezi kilichopo Wilayani Chato kilichojengewa kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.4 ambazo ni fedha za Tasaf.
Katika hatua nyingine Wajumbe hao wa kamati ya uongozi ya Tasaf wameshauri walengwa wa Tasaf waelimishwe ili watambue kuwa Umaskini sio sifa nzuri hivyo wanapaswa kutumia kidogo wanachopokea kwa malengo ili baada ya muda watoke kwenye lindi la umaskini na kujitegemea.