Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kwa kushirikiana na vyombo vingine likiwemo Jeshi la Polisi Manyara wameahidi kusaidia kutatua kero ya wanyama wakali kutishia maisha,kula mifugo na kuharibu mazao ya wananchi katika eneo la hifadhi ya Jamii ya wanyamapori ya Burunge (JUHIBU).
Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika Kijiji Cha Vilimavitatu kwa kuwashirikisha viongozi wa vijiji na wananchi,Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa TAWA Kanda ya Kaskazini ,Privatus Kasisi amesema Mamlaka hiyo, kwa kushirikiana na mamlaka nyingine wakiwepo wawekezaji wa utalii katika eneo hilo, Chemchem association watajitahidi kutatua kero hizo.
Amesema TAWA itajitahidi kuongeza magari ya doria na kufanya haraka kufika katika matukio yenye tishio la usalama katika eneo hilo lakini pia akitaka wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinaadamu ikiwepo kulima na kuingiza mifugo maeneo yaliyohifadhiwa kwani inawafanya wanyama kutoka hifadhini na kuvamia maeneo hayo.
Hata hivyo, alisema viongozi wa JUHIBU WMA, kwenda vijijini kupata takwimu za mahitaji ya vifaa vya Kupambana na uvamizi wa Wanyamapori, kwani taasisi yaChemChem ipo tayari kutoa vifaa ikiwepo Tochi, vuvuzela kufukuza wanyama na simu za mkononi ili viongozi waweze kutoa taarifa haraka wanapoona makundi ya wanyama wakali katika maeneo yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa Manyara,ACP George Katabazi, amesema jeshi hilo litaendelea kushirikiana na TAWA na vyombo vingi kuhakikisha usalama wa wananchi na kuwataka wananchi nao kuacha kujihusisha na vitendo vya ujangili.
Amesema Jeshi la Polisi Manyara kwa kushirikiana na TAWA watajitahidi kuitisha kikao kikubwa ambacho kitashirikisha viongozi wa TANAPA na Wizara ya Maliasili na Utalii ambao wanahusika na malipo ya fidia ili kumaliza migogoro katika eneo hilo,huku akiwataka Wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa kufichua uhalifu ikiwemo pia matukio ya ukatili wa kijinsia katika mkoa wa Manyara.
Wakazi wanaoishi katika eneo wameomba TAWA kuwasaidia kuwaondoa Fisi, Simba na Tembo katika makazi yao kwani wanatishia maisha na wamekuwa wakila mazao yao na mifugo huku wakiahidi kuwa wahifadhi na kuacha ujangili huko wakisema Kikao hicho kimekuwa ili kumaliza migogoro na kunaomba elimu ya uhifadhi iendelee kutolewa vijijini.