Ecuador imesema polisi wameondoa karibu miili 800 katika wiki za karibuni kutoka katika makazi mjini Guayaquil, sehemu iliyoathiriwa kwa kiasi kikubwa na mlipuko wa virusi vya corona, baada ya ugonjwa huo kuzidi uwezo wa huduma za dharura, hospitali na kampuni za mazishi.
Wafanyakazi katika vyumba vya kuhifadhia maiti katika mji huo wa pwani wamekuwa wakishindwa kukabiliana na vifo, huku wakazi wakituma video katika mitandao ya kijamii zinazoonyesha miili iliyotelekezwa mitaani.
“Idadi ya miili tuliyokusanya pamoja na kikosi maalum kutoka katika makazi inazidi maiti 700,” Jorge Wated, ambaye anaiongoza timu ya polisi na wanajeshi iliyoundwa na serikali kusaidia kukabiliana na athari za ugonjwa wa Covid-19.