Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limebaini mbinu wanazozitumia baadhi ya wafanyabiashara kuuza bidhaa ambazo zimepigwa marufuku katika soko la Tanzania hasa vipodozi na limesisitiza kutowafumbia macho wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Maofisa wa shirika hilo wamebaini mbinu hizo kwenye ukaguzi wa bidhaa sokoni katika Wilaya za Kasulu, Kibondo na Kakonko mkoani Kigoma kwa lengo la kuhakikisha bidhaa zote zinazouzwa sokoni zimekidhi matakwa ya kiwango husika.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa bidhaa hizo mkoani Kigoma mwishoni mwa wiki, Ofisa Usalama wa Chakula wa TBS, Elisha Meshack alisema ukaguzi huo umefayika kwenye maduka ya rejareja, jumla, kwa wasambazaji, supermarkets, migahawa na kwingineko na umeendana sambamba na kutoa elimu.
Alisema kwa sasa wamejua mbinu zao ambapo wapo wafanyabiashara wachache wasio waaminifu wanaoficha bidhaa zilizopigwa marufuku kwenye soko la Tanzania hasa vipodozi kwenye mabegi yao ya mkononi au katika ndoo za kuwekea uchafu dukani na endapo mteja anatokea basi anapatiwa bidhaa hiyo kwa kificho.
Meshack alifafanua kuwa TBS haitasita kuchukua hatua stahiki kwa wote watakaobainika kuuza bidhaa zilizopigwa marufuku, kwani ni kinyume cha sheria.
Alisema kwa kuwa mbinu wanazozitumia tayari zimebainika shirika hilo litahakikisha wafanyabiashara wachache wadanganyifu ambao wanauza bidhaa za vipodozi vilivyopigwa marufuku kwa kificho wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Hatutafumbia macho suala la wauzaji wa bidhaa ambazo zimepigwa marufuku hasa vipodozi,” alionya Meshack.
Alisema ukaguzi huo ni sehemu ya mkakati wa Shirika hilo kusimamia vyema majukumu yake kwa kuhakikisha ubora wa bidhaa na kulinda afya na usalama wa Watanzania na watumiaji wote.
“Tunafanya ukaguzi na kutoa elimu kwa wauzaji na wasambazaji wa bidhaa mbalimbali hasa za chakula na vipodozi ili kuhakikisha wananchi wanapatiwa bidhaa bora na salama,” alisema Meshack.
Wakizungumzia kuhusiana na ukaguzi huo, wananchi wengi waliunga mkono hatua hiyo ya TBS ya kufanya ukaguzi na kutoa elimu kwa umma, kwani kitendo cha wafanyabiashara kuuza kwa kificho bidhaa zilizopigwa marufuku ni kielelezo kuwa elimu imewafikia na wanajua kwamba wanavunja sheria.
“Tunafurahishwa na kazi inayofanywa na TBS, kwani hata watumiaji wa bidhaa za vipodozi sasa hivi wanajua ni vya aina gani havitakiwi kwenye soko la Tanzania, tunawapongeza kwa kazi kubwa,” alisema Joyce Edward, mkazi wa Kibondo.
Alisema ukaguzi huo utakuwa mwarobaini wa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiuza bidhaa za chakula na vipodozi zilizokwisha muda wa matumizi na vilevile kuuziwa vipodozi zenye viambata sumu.
Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Naftary Elisha, alisema; “Naishukuru TBS kwa kufika kwetu kwani kwa kufanya hivi ninaamini sisi wananchi tutaepukana na udanganyifu wa wauzaji sababu wanachukulia udhaifu wetu wa kutojua mambo au kutosoma na kutuuzia bidhaa ambazo hazina ubora na zilizokwisha muda wa matumizi, nashauri zoezi hili liwe endelevu ili tabia hii ya udanganyifu kwa wananchi ikome kabisa”.
TBS inaendelea na zoezi la ukaguzi wa bidhaa sokoni katika mikoa yote nchini, ambalo linaenda sambamba na usajili wa majengo yanayoshughulika na bidhaa za chakula na vipodozi ili kuhakikisha afya na usalama wa wananchi unalindwa.