Kwa mujibu wa Sheria Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imepewa jukumu la kusimamia maudhui yote yanayorushwa na vituo vya Utangazaji pamoja na mitandao ya ki-elektroniki.
Siku za hivi karibuni, kumekuwa na taarifa inayosambazwa na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya Kijamii ikitahadharisha juu ya uwepo wa maudhui ya televisheni kwenye vipindi vya watoto yaliyo kinyume na Sheria, Kanuni za Utangazaji, Maadili na Miiko ya utangazaji nchini.
TCRA ingependa kuuhakikishia umma kuwa vipindi vya maudhui vyote vinayorushwa na vyombo vya Utangazaji hapa nchini huhakikiwa kwanza na pia kufuatiliwa ili kujiridhisha kuwa yanazingatia Sheria, Kanuni, Maadili na Utamaduni wa Mtanzania.
TCRA imejiridhisha kuwa hakuna chombo cha Utangazaji kilichorusha maudhui hayo yasiyofaa kwa watoto. Hata hivyo, TCRA inavikumbusha Vyombo vyote vya Utangazaji kuendelea kuzingatia matakwa ya Sheria, Kanuni na Masharti ya Leseni ya Utangazaji kwa kuhakikisha vituo vyao haviendi kinyume na maadili ya kitanzania.
Aidha, TCRA inaendelea kusisitiza kuwa wajibu wa kuwalinda Watoto kutokana na maudhui yasiyofaa hasa kwenye mitandao ya kijamii ni wa kwetu sote ikianzia kwa Wazazi, Walezi na Mashuleni ambapo Watoto wetu hutumia muda mwingi huko wakiwa masomoni.
Pia TCRA inaiasa jamii kutosambaza katika mitandao ya kijamii jumbe zinazoleta taharuki, upotoshaji na hofu katika jamii. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale wote watakaobainika kusambaza jumbe hizo. TCRA inafuatilia kwa ukaribu maudhui yanayowekwa kwenye mitandao. Kwa yeyote atakayebainika kuweka na kusambaza habari za upotoshaji mitandaoni, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.