Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, ameongoza kikao muhimu na wazalishaji wadogo na wa kati wa mbolea nchini ili kujadili suala la utekelezaji wa takwa la sheria ya Mazingira la kufanya tathmini ya mazingira.
Katika kikao hicho kilicholihusisha Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kilifanyika tarehe 5 Februari, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka kikishirikisha wazalishaji wa mbolea wa viwanda 14 nchini.
Mkurugenzi Laurent aliwashukuru wazalishaji kwa kuitikia wito wa kikao hicho na kusisitiza kuwa TFRA ipo kwa ajili ya kuwezesha ukuaji wa viwanda vya mbolea nchini na si udhibiti pekee ili kuzalisha mbolea inayotosheleza mahitaji ya wakulima nchini.
“TFRA inalenga kuhakikisha viwanda vinazalisha mbolea bora inayokidhi viwango na kwamba Mamlaka hiyo iko tayari kuwasaidia wazalishaji kufanikisha hilo” Laurent aliongeza.
Ameeleza kuwa, katika kuhakikisha uzalishaji unafuata sheria na kanuni, TFRA inashirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kuhakikisha viwanda vinajengewa uwezo na kukidhi matakwa ya uhifadhi wa mazingira.
“Tumeona kuna changamoto ya uelewa kuhusu sheria hizi, ndiyo maana tumewaita wawakilishi wa NEMC ili kuwaelewesha na pia kupata maoni yeo,” alisema Bw. Laurent.
Pia, alieleza kuwa, TFRA inatafuta mbinu bora za kuhakikisha uzalishaji wa mbolea bora bila kuhitaji ukaguzi wa mara kwa mara, ili kurahisisha usimamizi wa viwanda na kuhakikisha uzalishaji unazingatia viwango vilivyowekwa.
Pamoja na hilo washiriki walieleza changamoto ya upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wazalishaji wadogo ambapo Bw. Laurent alieleza kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeonyesha utayari wa kuwapa wazalishaji mikopo kwa kiwango kinachohitajika huku ikishusha riba ili kupunguza mzigo wa kifedha kwa wawekezaji.
Naye Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani wa TFRA, Louis Kasera, aliwashauri wazalishaji kuunda kikundi chao na kuchagua kiongozi atakayeongoza hoja zao katika vikao mbalimbali na kusaidia mshikamano kati yao.
Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Temeke wa NEMC, Abel Sembeka, aliahidi kushughulikia changamoto zilizowasilishwa na kuweka mazingira rafiki kwa wazalishaji wadogo wa mbolea ili kukuza sekta hiyo nchini.
Awali,akielezea chimbuko la kikao hicho Kaimu Meneja Uzalishaji wa Ndani, Uhamasishaji na Mazingira, Getrude Ng’weshemi amesema, ni ziara waliyoifanya viwandani na kubaini changamoto zinazowakabili wazalishaji hao wa mbolea.
Amesema, ili kufikia lengo la kikao Mamlaka ililialika Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) ili kutoa mada na kuongoza mjadala wa kuwaelimisha washiriki kuhusu utekelezaji wa takwa hilo la kisheria.