Top Stories

TIRA kuhakikisha 80% ya wanafahamu juu ya bima, 50% watumie

on

Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),Taasisi ya Bima Tanzania (IIT) na Kikosi kazi cha Wataalamu (TWG) wamekuwa wenyeji katika sherehe za mahafali ya Wakufunzi waliofanikiwa kumaliza programu ya Mafunzo ya Wakufunzi (ToT) katika kozi ya msingi ya Huduma Ndogo za Bima.

Mafanikio ya mpango wa Mafunzo kwa Wakufunzi ni mwendelezo wa kazi kubwa iliyofanyika pamoja na kujitolea kwa kiwango cha juu kwa wabia yaani TIRA, IIT, IFM and FSDT ambao wapo mstari wa mbele katika kuenezaa ufahamu wa huduma ndogo za bima (microinsurance), kuongeza upatikanaji wake nchini, ili kuhakikisha kwamba lengo la kitaifa la huduma za bima kupenya kwa asilimia 50 kwa watu wazima ifikapo mwaka 2030 linafikiwa.

Kozi ya misingi ya huduma ndogo za bima ililenga kujenga uendelevu katika upatikanaji wa huduma za mafunzo huduma ndogo za bima Pamoja na upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi wa kiwango cha juu wa huduma ndogo za bima nchini Tanzania.

Walengwa wa mafunzo haya ni Maafisa waandamizi na wafanyakazi wataalamu kutoka katika makampuni ya bima, makampuni ya udalali na wasambazaji wanaojihusisha au wanaovutiwa na bisahara ya huduma ndogo za bima.

Kozi imeandaliwa ili kusaidia watendaji/wataalamu kupata, Uelewa wa mahitaji ya soko na namna ya kusaidia mteja kupata thamani ya huduma anayotumia; mikakati inayotumika kuhudumia soko la watu wa kipato cha chini kwa kuwapa bidhaa sahihi za bima; kuelewa makundi mbalimbali ya soko na mikakati inayolenga wateja wa huduma ndogo za bima; kuvumbua wigo wa huduma ndogo za bima na mifumo ya usambazaji; kujifunza machaguo yaliyopo katika kuunda mifumo ya huduma ndogo za bima na kubainisha vichocheo vya mafanikio Pamoja na changamoto zilizopo katika kufanikisha uhai wa thamani ya huduma ya bima kwa mteja.

Wakati wa wa sherehe hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa FSDT, Sosthenes Kewe, amesema “Mpango wa Mafunzo kwa wakufunzi ni mpango maridadi na ubunifu mkubwa unahusisha mafanikio yake na ushirikiano baina ya sekta binafsi na serikali (PPP) kupitia Hati ya Makubaliano (MoU)”

“Pamoja na utayari wa kujitolea wa sekta ya bima kuchukua jukumu la makusudi kuhusika na kuleta thamani kutoka kwenye nyenzo zilizotolewa kupitia kozi hii. FSDT inajivunia kuwa sehemu ya mpango huu kama mdau wa maendeleo kwasababu tunaona kukamilika kwa mpango wa mafunzo kwa wakufunzi (ToT) kama hatua kubwa na ya uhakika ambayo wadau wote wa sekta ya bima wameikubali.“ Sosthenes Kewe

Programu ya Mafunzo ya Wakufunzi (ToT) ilihusisha usaili wa kubaini vigenzo vya awali vya wakufunzi, hatua ya kudahili na kuorodhesha,kuwezesha kuendesha kozi kwa Pamoja kati ya mkufunzi na Mkufunzi Mkuu, kumalizia uchambusi wa maandishi, na mwisho kabisa kuendesha kozi bila kusaidiwa na washirika ambao walisaini na kulipia gharama ya kuhudhulia mafunzo, wakati Mkufunzi mkuu akiangalia.

Mkuu wa Kitengo cha Bima na Ulinzi wa Watumiaji, Bi. J. Kemibaro Omuteku, aliongezea, “Tunawapongeza wakufunzi tisa ambao wamefuzu kama wakufunzi wa kozi ya msingi ya Huduma Ndogo za Bima.Wakufunzi ni watendaji wa tasnia na wasomi katika sekta ya bima. Tumefurahishwa sana na mafanikio ya wakufunzi wanaohitimu leo, kwani wote wamefanya kazi kwa juhudi kubwa na wamepitia hatua kadhaa ili kuhitimu kama wakufunzi.”

Kaimu Mkurugenzi wa Sheria wa TIRA akizungumza kwa niaba ya Mamlaka ya Udhibiti wa Bima nchini, Emily Kiria, amesema, “TIRA inachukua jukumu la uratibu wa soko ili kuhakikisha kuna mazingira mazuri yanayowezesha utekelezaji wa lengo la kitaifa kuwa na angalau 50% ya watu wazima wanaotumia angalau bidhaa moja ya bima”

“80% ya watu wote wawe na ufahamu kuhusu huduma za bima; huduma za bima zinazolenga watuamiaji ziwepo sokoni; na kuwe na njia bora za kushughulikia madai ya watuamiaji wa huduma za bima, ili kuongeza uaminifu katika tasnia ya bima. Yote haya yawe yamekamilika ifikapo mwaka 2030. Zaidi ya hayo, TIRA imezindua mfumo mpya wa kushughulikia bima ya magari kuanzia tarehe 01/4 / 2021.” Emily Kiria

Mkuu wa IFM, Prof. Tadeo Satta, alisema, “Kama moja ya taasisi zinazoongoza katika kutoa mafunzo ya taaluma ya fedha, tunafurahi kupata nafasi ya kufanya kazi pamoja na TIRA, FSDT na IIT. Uhusiano wetu na IIT ni uhusiano wenye faida pande zote. Tutaendelea kufanya kazi pamoja ili kukuza kozi ya Msingi ya Bima Ndogo, kutatua pengo la ujuzi katika bima hii, na kuhakikisha uendelevu wa kozi hiyo. ”

Rais wa IIT, Bw. Bosco Bugali, alisema kuwa sekta ya bima ilikuwa imeweka kipaumbele katika malengo nane ya bima ndani ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/2021 hadi 2029/2030. “Malengo ya kozi ya Msingi ya Bima Ndogo yanashabiiana na malengo ya kujenga uwezo wa sekta ya fedha, kama vile kuinua kiwango cha huduma za fedha jumuishi na kuhakikisha kuna ulinzi wa watumiaji wa huduma za fedha.”

Mwakilishi wa Chama cha Makampuni ya Bima Tanzania (ATI) na Kikosi Kazi cha Utaalamu wa Tasnia ya Bima Ndogo (TWG), Bi. Neema Kaaya, alisema, “ATI na TWG zinajumuisha wadau wengi katika sekta ya bima. Vyombo vyote viwili vinaunga mkono mpango wa programu ya Mafunzo ya Wakufunzi (ToT) kwa sababu unaendana na malengo makuu ya sekta ya bima nchini na utekelezaji wake.”

Soma na hizi

Tupia Comments