Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA ) Mkoa wa Geita imesema kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2020/21 walikuwa na ongezeko la Mapato kwa Asilimia 67 ukilinganisha na Lengo walilojiwekea kukusanya kwa kipindi hicho.
Akizungumza katika Maonyesho ya 5 ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Bombambili Mkoani Geita, Meneja Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Geita, Hashimu Ngoda kwa mwezi ulioisha walikuwa na lengo la kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 3.1 ambapo mpaka mwisho wa Mwezi wamekusanya kiasi cha shilingi Bilioni 3.9 ambayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 124.
“Kwa hiyo Geita tunakwenda Vizuri kwa mwezi tuu wa kipekee wa 9 tuliotoka kuumaliza ambao tulikuwa na lengo la kukusanya Bilioni 3.1ambapo hadi mwisho wa mwezi tulikusanya kiasi cha shilingi Bilioni 3.9 ambao ni sawa na ufanisi wa asilimia 124,” Meneja TRA Mkoa wa GEITA.
Aidha Ngoda amesema kwa kipindi hiki cha Mwaka wa Fedha wa 2021/22 Mkoa wa Geita walikuwa na lengo la kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 8.9 mpaka wanamaliza robo ya mwaka wameshafikia lengo la Makusanyo ya Bilioni 11.9 ambao ni sawa na wastani wa ufanisi wa Asilimia 132 ya lengo walilopewa.
Ngoda ameendelea kusema kwa kuwashukuru wanageita kwa kuendelea kulipa kodi katika kuhakikisha mkoa wa Geita unafanya vizuri katika makusanyo ya kodi ya Serikali huku akiahidi kuzifanyia kazi changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo.