WAKATI maadhimisho ya wiki kwa mlipa Kodi yakikaribia kufikia kilele chake, Januari 23, 2025, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeandaa bonanza litakalowakutanisha wafanyabiashara wa Kariakoo na wafanyakazi wa TRA ili kuendelea kujenga mahusiano mazuri baina yao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bonanza hilo leo Januari 16,2025 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka wafanyabiashara hao kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya kidongo chekundu ili kushiriki katika bonanza hilo kwani mbali na bonanza pia watapata wasaa wa kuzungumza na kujadiliana na Kamishna Mkuu wa TRA katika masuala mbali mbali ya kodi.
Bonanza hilo litakalofanyika Jumapili Januari 19, 2025 litajudhuriwa na Mkuu wa Wilaya Mpogolo pamoja na
vikundi vya jogging wilayani humo ikiwa ni mwendelezo wa wiki ya mlipa kodi.
“Bonanza hili limelenga kujenga mahusiano mazuri na TRA pamoja na kusema asante kwa kuendelea kulipa kodi, bonanza la kwanza lilisaidia watu kujua afya zao na hata kuondoa woga kati ya wafanyabiashara na Mamlaka, kwa sasa bonanza linaendelea kufanyika kwa ukubwa zaidi,”amesema Mpogolo.
Amesema bonanza hilo litaaanza kwa kutembea umbali wa Kilometa tano katika eneo la Kariakoo na kuhitimishwa kidongo chekundu ambapo kutakuwepo na michezo ya kuvuta kamba, kukimbia na magunia, kukimbiza kuku, na kukimbia na yai kwenye kijiko.
Pia Mpogolo amewataka wafanyabiashara wote kushiriki bonanza hilo kwani watapata fursa ya kutafakari mambo makubwa yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha uongozi wake tangu ameingia madarakani.
Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Kariakoo,Severin Mushi amewahimiza wafanyabiashara kuitumia siku hiyo kama fursa ya kuzungumza na Kamishina Mkuu ili kuendelea kupata elimu pale wanapoona hapakueleweka.
“Jitokezeni kwa wingi hata kama kwa sasa tumeandaa bonanza hili kwa muda mfupi lakini wakati ujao tutaandaa vizuri kwa kuzingatia zawadi kwa washiriki wote” amesema