Kampuni ya Uwakala wa Usafiri Mtandaoni ya Trip.com Group imesema itaanza kumlipa kila Mfanyakazi wake Yuan 50,000 (Tsh. Mil 16.6) kwa kila Mtoto mmoja atakayempata kuanzia July 01,2023 hii ikiwa ni Kampuni ya kwanza binafsi kuonesha jitihada za kuunga mkono mapambano ya China kuongeza Watoto na kupunguza uwingi wa Wazee ambao sio Wazalishaji mali.
Kampuni hiyo yenye Watumiaji zaidi ya Mil 400 Duniani, imesema licha ya kumpa Mzazi Yuan 50000 mara tu akipata Mtoto, italipa pia Yuan 10000 (Mil 3.3) ya matunzo ya Mtoto kila mwaka kwa muda wa miaka mitano kwa kila Mfanyakazi wa Kampuni hiyo atakayepata Mtoto popote Duniani ambapo Kampuni inakadiria kutumia Yuan Bil 1 kwenye programu hiyo.
Kiongozi wa Kampuni hiyo James Liang amesema “Siku zote huwa nashauri Serikali iwape pesa Wazazi hususani wenye Watoto wengi ili kuwahamasisha Vijana kutimiza ndoto za kuwa na Watoto wengi”
China ambayo iliendesha sera ya kila Mzazi kuwa na Mtoto mmoja pekee kuanzia 1980- 2025 imeonywa na Wataalamu kuwa ‘Nchi Itazeeka kabla ya kutajirika’ kutokana na nguvu kazi ya Taifa (Vijana) kupungua na kuwa na Wazee wengi ambao wanahitaji kuhudumiwa zaidi ambapo kuanzia mwaka 2021 wamefungua milango na kuruhusu Watu kuzaliana hadi Watoto watatu ingawa bado Watu wamegoma kuzaliana wakihofia gharama za matunzo ya Watoto, ada, kipato duni n.k.
Kiwango cha kuzaliana China kimeshuka hadi vizazi 6.77 kati ya Watu 1000 kutoka 7.52 kati ya Watu 1000 mwaka 2021 ambapo Wataalamu wanasema 2% ya GPD ya China itategemea kuhamasisha Watu kuzaliana.